Swahili New Testament Bible

Luke 12

Luke

Return to Index

Chapter 13

1

Wakati huo watu fulani walikuja, wakamweleza Yesu juu ya watu wa Galilaya ambao Pilato alikuwa amewaua wakati walipokuwa wanachinja wanyama wao wa tambiko.

2

Naye Yesu akawaambia, "Mnadhani Wagalilaya hao walikuwa wahalifu zaidi kuliko Wagalilaya wengine, ati kwa sababu wameteseka hivyo?

3

Nawaambieni hakika sivyo; lakini nanyi, hali kadhalika, msipotubu, mtaangamia kama wao.

4

Au wale kumi na wanane walioangukiwa na mnara kule Siloamu wakafa; mnadhani wao walikuwa wakosefu zaidi kuliko wengine wote walioishi Yerusalemu?

5

Nawaambieni sivyo; lakini nanyi msipotubu, mtaangamia kama wao."

6

Kisha, Yesu akawaambia mfano huu: "Mtu mmoja alikuwa na mtini katika shamba lake. Mtu huyu akaenda akitaka kuchuma matunda yake, lakini akaukuta haujazaa hata tunda moja.

7

Basi, akamwambia mfanyakazi wake: `Angalia! Kwa miaka mitatu nimekuwa nikija kuchuma matunda ya mtini huu, nami nisiambulie kitu. Ukate! Kwa nini uitumie ardhi bure?`

8

Lakini naye akamjibu: `Bwana, tuuache tena mwaka huu; nitauzungushia mtaro na kuutilia mbolea.

9

Kama ukizaa matunda mwaka ujao, vema; la sivyo, basi utaweza kuukata."`

10

Yesu alikuwa akifundisha katika sunagogi moja siku ya Sabato.

11

Na hapo palikuwa na mwanamke mmoja aliyekuwa mgonjwa kwa miaka kumi na minane kutokana na pepo aliyekuwa amempagaa. Kwa sababu hiyo, mwili wake ulikuwa umepindika vibaya hata asiweze kusimama wima.

12

Yesu alipomwona, alimwita, akamwambia, "Mama, umeponywa ugonjwa wako."

13

Akamwekea mikono, na mara mwili wake ukawa wima tena, akawa anamtukuza Mungu.

14

Lakini mkuu wa sunagogi alikasirika kwa sababu Yesu alikuwa amemponya siku ya Sabato. Hivyo akawaambia wale watu walikusanyika pale, "Mnazo siku sita za kufanya kazi. Basi, fikeni siku hizo mkaponywe magonjwa yenu; lakini msije siku ya Sabato."

15

Hapo Bwana akamjibu, "Enyi wanafiki! Nani kati yenu hangemfungua ng`ombe au punda wake kutoka zizini ampeleke kunywa maji, hata kama siku hiyo ni ya Sabato?

16

Sasa, hapa yupo binti wa Abrahamu ambaye Shetani alimfanya kilema kwa muda wa miaka kumi na minane. Je, haikuwa vizuri kumfungulia vifungo vyake siku ya Sabato?"

17

Alipokwisha sema hayo, wapinzani wake waliona aibu lakini watu wengine wote wakajaa furaha kwa sababu ya mambo yote aliyotenda.

18

Yesu akauliza: "Ufalme wa Mungu unafanana na nini? Nitaulinganisha na nini?

19

NI kama mbegu ya haradali aliyotwaa mtu mmoja na kuipanda shambani mwake; ikaota hata ikawa mti. Ndege wa angani wakajenga viota vyao katika matawi yake."

20

Tena akauliza: "Nitaulinganisha Ufalme wa Mungu na nini?

21

Ni kama chachu aliyoitwaa mama mmoja na kuichanganya pamoja na unga debe moja kisha unga wote ukaumuka wote."

22

Yesu alindelea na safari yake kwenda Yerusalemu huku akipitia mijini na vijijini, akihubiri.

23

Mtu mmoja akamwuliza, "Je, Mwalimu, watu watakaookoka ni wachache?"

24

Yesu akawaambia, "Jitahidini kuingia kwa kupitia mlango mwembamba; maana nawaambieni, wengi watajaribu kuingia lakini hawataweza.

25

"Wakati utakuja ambapo mwenye nyumba atainuka na kufunga mlango. Ninyi mtasimama nje na kuanza kupiga hodi mkisema: `Bwana, tufungulie mlango.` Lakini yeye atawajibu: `Sijui mmetoka wapi.`

26

Nanyi mtaanza kumwambia: `Sisi ndio wale tuliokula na kunywa pamoja nawe; na wewe ulifundisha katika vijiji vyetu.`

27

Lakini yeye atasema: `Sijui ninyi mmetoka wapi; ondokeni mbele yangu, enyi nyote watenda maovu.`

28

Ndipo mtakuwa na kulia na kusaga meno, wakati mtakapowaona Abrahamu, Isaka na Yakobo, na manabii wote wapo katika Ufalme wa Mungu, lakini ninyi wenyewe mmetupwa nje!

29

Watu watakuja kutoka mashariki na magharibi, kutoka kaskazini na kusini, watakuja na kukaa kwenye karamu katika Ufalme wa Mungu.

30

Naam, wale walio wa mwisho watakuwa wa kwanza; na wale walio wa kwanza watakuwa wa mwisho."

31

Wakati huohuo, Mafarisayo na watu wengine walimwendea Yesu wakamwambia, "Ondoka hapa uende mahali pengine, kwa maana Herode anataka kukuua."

32

Yesu akawajibu, "Nendeni mkamwambie huyo mbweha hivi: `Leo na kesho ninafukuza pepo na kuponya wagonjwa, na siku ya tatu nitakamilisha kazi yangu.`

33

Hata hivyo, kwa leo, kesho na kesho kutwa, ni lazima niendelee na safari yangu, kwa sababu si sawa nabii auawe nje ya Yerusalemu.

34

"Yerusalemu! We Yerusalemu! Unawaua manabii na kuwapiga mawe wale waliotumwa kwako! Mara ngapi nimetaka kuwakusanya watoto wako pamoja kama kuku anavyokusanya vifaranga vyake chini ya mabawa yake, Lakini wewe umekataa.

35

Haya, utaachiwa mwenyewe nyumba yako. Naam, hakika nawaambieni, hamtaniona mpaka wakati utakapofika mseme: `Abarikiwe huyo ajaye kwa jina la Bwana."`

Luke 14

 

 

 

Please Click the Ads.

Clicking the Ads helps us to keep this free Bible website open for everyone.

Thanks!

 

 

 

HTMLBible Software - Public Domain Software by johnhurt.com

 


Other Items are Available At These Sites: